Mhubiri
Mlango 11
Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi.
2 Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane; Maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
3 Mawingu yakiwa yamejaa mvua, Yataimimina juu ya nchi; Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.
4 Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5 Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.
6 Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa, kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa.
7 Kweli nuru ni tamu, tena ni jambo la kupendeza macho kutazama jua.
8 Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Mambo yote yajayo ni ubatili.
9 Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.
10 Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.