0:00
0:00

Mlango 1

Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,
2 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi;
3 Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu.
4 Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu.
5 Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya Bwana, iliyoko Yerusalemu.
6 Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu.
7 Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya Bwana, alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu ,na kuvitia katika nyumba ya miungu yake.
8 Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda.
9 Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu, visu ishirini na kenda.
10 mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu.
11 Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.