Uhuru kutoka Hofu

0:00
0:00

 • Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. Zaburi 27:1, 5
 • Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote. Zaburi 34:4
 • Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya. Mithali 1:33
 • Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Isaya 35:4
 • usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Isaya 41:10
 • Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Warumi 8:15
 • Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. 2 Timotheo 1:7
 • Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Zaburi 46:1-3
 • Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe; Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini? Zaburi 56:3, 4
 • Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Zaburi 91:5, 6
 • Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu. Mithali 3:24
 • Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. Yeremia 1:8
 • Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo. 1 Yohana 4:18
 • Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Waebrania 13:5, 6
 • Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Yohana 14:27
 • Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Waebrania 2:14, 15